TEKNOLOJIA YARAHISISHA UREJESHAJI WA MAKUNDI MANNE YA TEMBO MAENEO YA HIFADHI

Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia taasisi zake TAWIRI, TANAPA na TAWA imeendelea kutekeleza jukumu la kutatua migongano baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu nchini hususani tembo.

Akizungumza wakati wa zoezi la kuyarejesha makundi ya tembo hifadhini, Wilayani Bunda, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAWIRI Dkt. Emmanuel Masenga ambaye pia ni Mtafiti Mkuu na Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Wanyamapori Serengeti, amesema TAWIRI imeendelea kutumia teknolojia ya helikopta na uvishaji wa mikanda yenye redio za mawasiliano (GPS Satellite Collar) ili kurahisisha kufuatilia mienendo ya tembo na kuwadhibiti pindi wanapotoka hifadhini kabla ya kuingia kwenye makazi ya wananchi.

Dkt. Masenga amesema katika zoezi hilo wamefanikiwa kutumia helikopta kurejesha makundi manne yenye jumla ya tembo 90 katika hifadhi ya Taifa Serengeti, Pori la Akiba Kirejeshi na Grumeti sambamba kumvalisha GPS satellite collar tembo jike ambaaye ni kiongozi wa kundi lenye tembo 12

Aidha, Dkt. Masenga amesema zoezi la kuwarejesha tembo kwa kutumia teknolojia ya helikopta na kuvalisha GPS satellite collar ni endelevu na limefanyika katika Wilaya za Ruangwa, Nachingwea, Liwale, Same na Mwanga.

Dkt. Masenga amebainisha kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu karibu na maeneo ya hifadhi kumechochea tembo kutoka nje ya hifadhi na kuingia kwenye makazi ya wananchi ambapo awali yalikuwa yanatumiwa kama mapito ya tembo, hivyo ametoa rai kwa jamii kuacha kuendesha shughuli za kibinadamu katika maeneo hayo ili kupunguza migongano.

Vilevile Dkt.Masenga ameitaka jamii kushiriki kikamilifu katika utatuzi wa migogoro pindi tembo wanapoingia kwenye makazi ya wananchi kwa kutoa taarifa kwa vikosi vya askari wa wanyamapori vinavyosimamiwa na TANAPA na TAWA.

Visitors

013719
Users Today : 45
Users Last 7 days : 371
Users This Month : 711
Total Users : 13719

Office Location

Contact Us