TAWIRI yashiriki Maadhimisho ya Siku ya Misitu Duniani yaliyoanza tarehe 18 Machi na yatakayofikia kilele tarehe 21 Machi, 2026 katika Viwanja vya Ilulu Mkoani Lindi
Katika Maadhimisho haya Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) imeonesha nafasi ya wadudu wachavushaji (nyuki, vipepeo n.k.) katika kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula, pamoja na mchango wa wadudu katika uendelevu wa misitu, ikiwemo mende wanaokula kinyesi (dung beetles) ambao kwa kuviringisha kinyesi huchangia kusambaza mbegu na kurutubisha udongo hivyo kusaidia uoto mpya wa misitu.
Maonesho pia yameangazia umuhimu wa asali ya nyuki wasiodunga (stingless honey) yenye sifa za kupambana na bakteria, kuimarisha kinga ya mwili na kusaidia uponyaji wa vidonda pamoja na matatizo ya ngozi. Vilevile, matumizi ya mimea vamizi kutengeneza briketi yanaoneshwa kama suluhisho la nishati mbadala linalopunguza utegemezi wa kuni na mkaa hivyo kuchangia uhifadhi wa misitu.
Aidha, mmea Aristida adscensionis (maarufu kama nyasi ya miiba mitatu au Sixweeks Threeawns) umeoneshwa kwa mchango wake katika uhifadhi wa ardhi na uoto wa asili, ukithibitisha kuwa misitu ni msingi wa uchumi na maendeleo endelevu ya Taifa.



